Blog hii inalenga kumjulisha Mtanzania juu ya masuala yanayohusu Kilimo na Ufugaji bora kwani watu wengi bado hawajapata elimu ya kutosha juu ya kilimo na ufugaji bora, Kwani Kilimo ni fursa kubwa ya kiuchumi katika ulimwengu huu wa leo, tembelea blog hii ili kujifunza kwa undani kuhusu fursa zinazopatikana kupitia kilimo.
advert
Friday, August 24, 2012
Sunday, August 19, 2012
Friday, August 10, 2012
KILIMO CHA UMWAGILIAJI
Fri 10 Aug 7:23AM
Kina mama wavutiwa na kilimo cha umwagiliaji kilombero
|
Thursday, 26 July 2012 10:59
|
MRADI mkubwa wa umwagiliaji katika Kijiji cha Mkula umeonekana kuwaletea manufaa wakazi wa kijiji hicho na vijiji vya jirani baada ya uzalishaji wa mpunga kuongezeka.
Mradi wa umwagiliaji una ukubwa wa hekta 254 na umebadilisha maisha ya wakazi wa vijiji hivyo kwa mfano, njaa sasa itakuwa ni historia.
Mradi huo uko chini ya Mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo wilayani Kilombero (DAADP’S) na umeweza kuboresha maisha ya wakulima hao baada ya mavuno kuongezeka.
Kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo wakulima walikuwa wakivuna magunia matano ya mpunga katika heka moja, lakini sasa wanapata gunia 20 mpaka 25—matokeo ambayo yamewavutia watu wengi hasa vijana kujiingiza kwenye kilimo tofauti na awali.
“Tunaishukuru Wilaya ya Kilombero kwa kutuletea mradi huu kwani suala la njaa kwa sasa halipo pia tuna uwezo wa kuwasomesha watoto bila shida baada ya kuuza mazao yetu,”anasema Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkula, Salehe Semboko.
Mradi huo ambao ulianza mwaka 2005 umewavutia vijana ambao awali walikuwa hawapendi kulima kwa kuwa kazi hiyo haikuwa na faida.
Lakini kuanzishwa kwa mradi huo umebadilisha mtazamo wa vijana na wameamua sasa kuanzisha shughuli za kilimo kwa kuwa wanavuna mazao mengi na kuyauza.
“Hapa kwetu tuna misimu mitatu ya kilimo kwa mwaka ukilinganisha na maeneo mengine, hii imesababisha tujitume zaidi—mpaka sasa asilimia 80 ya vijana wetu wanajishughulisha na kilimo,” anafafanua mkulima kijana, Mohamed Nafulisa.
Wanawake nao hawako nyuma wanasema kipato chao kimeongezeka na wana uwezo wa kuendesha familia zao baada ya mavuno kuongezeka na kufanikiwa kuwasomesha watoto wao bila tatizo. “Kwa kiasi kikubwa mradi huu umetutoa katika umasikini, mimi nilikuwa naishi Dar es Salaam, lakini baada ya kuja huku na kuona wanawake wengine wanavyofaidika na mradi nikaamua kuanza kulima, sasa nasomesha watoto wangu mimi mwenyewe,” mkazi wa Kijiji cha Mkula, Dora Manyema. Pamoja na mradi huo kuboresha maisha ya wakazi wa Mkula bado wakulima hao wanakabiliwa na matatizo mengi kwa mfano kuna baadhi ya maeneo hayafikiwi na maji. Kutokana na kuwapo kwa tatizo hilo hekta 100 tu zinafikiwa maji huku hekta 154 zikiwa hazina maji na kusubiri mvua. Matatizo mengine wakulima wengi hawana pembejeo hasa mbolea ambayo haifiki kwa wakati na kukosa dawa ya kuulia wadudu hivyo kuwapa wakati mgumu wakulima hao.
“Unajua suala la mbolea kuchelewa linatutatiza sana kwa mfano, tunakuwa na mahitaji ya mbolea na pembejeo nyingine Oktoba, lakini zinafika hapa Aprili sasa tutazitumia vipi? Anahoji Semboko.
Tatizo lingine linaloonekana kuwakwamisha wakulima hao ni kutopatiwa mafunzo ya kuaandaa mashamba, kupalilia, kuvuna, kutafuta masoko.
Tatizo la wakulima kutopatiwa mafunzo—limesababisha wakulima kuuza mazao yao kwa bei ambayo inawanufaisha wafanyabiashara kutokana na madalali kupanga bei zao.
Wakulima hao wanazimika kuuza mazao yao kwa kufuata bei ya madalali kwa sababu hawajui soko la kuuzia mazao yao. Suala la mbolea feki limeonekana kuwatesa wakulima wa Kijiji cha Mkula kutokana na ukweli kwamba wanatumia gharama nyingi kuhakikisha wanapata mbolea kwa ajili ya mavuno yenye tija, lakini wanaambulia kupata mbolea feki ambayo imekuwa ikiharibu mazao yao. “Kwa mfano tulitumia mbolea, lakini baada ya siku chache mazao yalibadilika rangi na kuwa njano tupu na kudhoofika, kwa sasa tunataka mbolea ikabidhiwe kwetu moja moja, kuliko mbolea kupitia kwa mwakala,” anaelezea Dora Abdallah. Kukosekana kwa mashine ya kukoboa imekuwa tatizo kubwa kutokana na kuwapo kwa mashine chache na wakulima wamekuwa wakitumia gharama kubwa na muda mwingi kufuata huduma hiyo mbali na kijiji hicho. Wakulima hao wanaamini kwamba kama wafanyabisahara watafunga mashine za kukoboa wataweza kukoboa mchele na kuuza na thamani ya bidhaa hiyo kuongezeka. “Kama wawekezaji watajitokeza na kuwekeza kwenye pembejeo itasaidia kuongeza uzalishaji, pia naamini watu wengine watatamani kushiriki katika kilimo kwani kwa sasa kilimo ni biashara,” anasema Abdallah. Wakulima wanaiomba Serikali, taasisi binafsi na wadau mbalimbali kuiangalia Kijiji cha Mkula kwa jicho la tofauti kwa kuwa wanaamini kama matatizo ya pembejeo, masoko yatatatuliwa, ghala la chakula la Taifa litapata chakula kingi kutoka katika kijiji hicho. “Siyo maeneo mengi yana uwezo wa kuzalisha kwa misimu mitatu, lakini hapa kwetu hilo linafanyika basi ni wakati mzuri wa kuweka utaratibu mzuri wa kutufikishia pembejeo kwa wakati. Wakulima hao wanashauri kwamba wanaoshughulikia masuala ya pembejeo wanapaswa kuzungumza na wa wakulima hao ili kujua mahitaji yetu,” anasisitiza mwenyekiti wa Kijiji cha Mkula, Semboko. Wakulima wa kijiji hicho wanabainisha kwamba kutokana wao kufanikiwa kuzalisha mpunga kwa misimu mitatu, wakulima wa maeneo mengine wanapaswa kujifunza mengi kutoka kwao ili wafanikiwe katika kilimo cha mazao mbalimbali.. |
Thursday, August 9, 2012
Hilo ni shamba la mpunga ni huko mang'ula kilombero
SRI MFUMO WENYE TIJA KATIKA KILIMO CHA MPUNGA
Stella Mwaikusa
SRI MFUMO WA KUZALISHA MPUNGA KWA TIJA ZAIDI
Sekta ya kilimo ni sekta mhimu sana katika kuleta maendeleo kwa nchi yeyote duniani kwani mataifa mengi tunayoyaona na kuyaita mataifa ya ulimwengu wa kwanza yamefika hapo kutokana na sera nzuri za kilimo katika mataifa yao.
Hapa kwetu asilimia kubwa ya watanzania ni wakulima hii inaonyesha kuwa ipo haja kubwa ya kuweka nguvu nyingi kuhakikisha kuwa sekta hii mhimu inakuwa endelevu katika maeneo yote yaani kupatikana kwa pembejeo kwa wakati, kuwepo kwa viwatilifu, wakulima wapatiwe elimu ya kutosha kuhusiana na kilimo bora pamoja na uhakika wa masoko ya mazao yao.
Tukizungumzia mazao ya chakula katika nchi yetu hatuwezi kuliacha zao la mpunga ambalo limekuwa mkombozi kwa wakulima wa maeneo mbalimbali kwani pamoja na kuwa zao la chakula zao la mpunga limekuwa ni msaada mkubwa kwa pato la kaya.
Pamoja na umhimu wa zao hili bado kumekuwa na uzalishaji usioridhisha kutokana na matatizo mbalimbali ikiwa na ni pamoja na kukosekana kwa mbegu bora, wakulima kutumia njia isiyofaa hasa katika upandikizaji wa miche, kukosekana kwa mbolea ya kupandia pia matumizi ya maji mengi kwenye mashamba kwa kipindi chote cha ukuaji wa mpunga.
Kutokana na kuwepo kwa matatizo hayo Afisa kilimo wa mkoa wa Iringa bwana Shalimwene Kombo Ndondole anaelezea kuwepo kwa mfumo mpya na bora wa kulima mpunga ambao anaamini utaleta tija kwa wakulima iwapo watautumia kikamilifu.
Mfumo huu mpya ambao unajulikana kama SRI ikiwa ni kifupisho cha (System of Rice Intensification) ni njia iliyoboreshwa katika uzalishaji wa mpunga na iliasisiwa mwaka 1983 huko Madagascar kwa sasa mfumo huu wa umesambaa na kutumiwa sehemu mbalimbali duniani.
“Kuna imani kwamba Teknolojia na utafiti uliofanywa kupitia vishamba vidogo vya majaribio na kutoa kanuni bora inayofaa kwa kilimo cha mpunga ilibuniwa na wakulima wenyewe hivyo wakulima wa kitanzania pia wanapaswa kuwa wanasayansi watafiti” anafafanua Bwana Ndondole.
Ndondole anasisitiza kuwa wakulima wasiwe tu watu wa kufuata yaliyoshauriwa bali ni vema kuzielewa kanuni za uzalishaji na kuzitumia kulingana na mazingira na mahali kulingana na raslimalizilizopo kwani hii ndio kanuni mhimu katika kutumia mfumo wa SRI katika kilimo cha mpunga.
Nayo taasisi ya Rular urban development Initiatives (RUDI) inatoa elimu hii ya SRI yaani mfumo bora wa kilimo cha mpunga kwa vikundi mbalimbali vya wakulima kwa kuwatumia wataalam wa kilimo ili kuhakikisha kuwa kilimo cha mpunga kinakuwa chenye tija hivyo kusisitiza umhimu wa kutumia mbegu bora ya mpunga.
Meneja mradi wa Rudi wilaya ya kilombero Mang’ula anawataka wakulima kutumia mfumo huu mpya kutokana na ukweli kwamba SRI ni mfumo unaotumia maji kidogo hivyo hii ni nafasi ya kipekee kwa wakulima wa kitanzania hasa wanaoshi sehemu yenye uhaba wa maji.
Pamoja kuwahamasisha wanavijiji wa Mkasu, Mang’ula, na Katurukila meneja mradi huyo wa Rudi anasisitiza umhimu wa kutumia mbegu bora kwani anaamini kuwa mbegu bora ni moja ya kanuni inayoshauriwa na wataalamu wa kilimo kwani kwa kufanya hivyo wakulima watapata mavuno mara dufu
“Zipo aina kadhaa za mbegu bora lakini TXD306 (SARO) Imeonekana kuwa mbegu bora kwani hairefuki , inatoa machipukizi mengi, na ina uwezo wa kutoa mavuno gunia 30 na zaidi kwa eka moja zenye uzito kilo 80 kwa kila moja” anafafanua bwana Mghonu na kuongeza kuwa mbegu hii ya SARO hutoa mchele mzuri unaonukia vizuri sifa ambayo inaifanya iwe na soko kubwa lakini pia hakuacha kueleza mbegu za asili zinazofaa akizitaja kuwa ni kilombero, Faya, Indiarangi yaani rangi mbili pamoja na wahiwahi.
Wakulima wa kijiji cha mkasu wanaonekana kuufurahia mfumo huu mpya kwani wanaamini kuwa kuwepo kwa mfumo usiohitaji maji mengi utawafanya wazalishe kwa tija kwani hawategemea mvua tu kwani maji kidogo yatakayopatikana yatatosha kuzalisha kwa wingi kwani tayari wamekwisha pata elimu namna ya kupanda kitaalam kupitia mfumo wa SRI.
“Elimu ya mfumo huu usiotumia maji mengi umetupa matumaini mapya katika kilimo chetu cha mpunga kwani siku zote tumekuwa tukihitaji elimu juu ya kilimo lakini kwa sasa naona taasisi hii ya RUDI imesikia kilio chetu” anaeleza Abasi Likamu mkulima wa mpunga katika kijiji cha mkasu.
Afisa kilimo wa mkoa wa Iringa bwana Ndondole anasema mfumo huu wa SRI kwa sasa upo katika majaribio katika wilaya za Kilosa, Mvomero na Kilombero ili kuona namna mfumo huu utakavyotumika kwa nchi nzima, lakini pia amewaomba wakulima kuupokea mfumo huu kwani anaamini kuwa utaleta tija.
“Kwa kuwa mfumo huu wa SRI ni mpya basi nashauri wakulima waweze kuona tofauti kati ya mfumo huu na wazamani kwa kuwatumia wataalam wa mashamba darasa ambao ni lazima waonyeshe kwa vitendo kwa kuwa na plot mbili moja ipandwe kwa mfumo huu wa SRI na nyingine kwa mfumo wa kizamani ili kuwathibitishia wakulima” anafafanua bwana Ndondole.
Pamoja na kuelezea namna mfumo huo unavyoweza kuleta tija kwa wakulima wa mpunga bwana ndondole aliwataka wataalam wa shamba darasa wawe wabunifu katika kuhakikisha kuwa wanajaribu na kuzikubali mbinu mpya za kilimo ili kuboresha maisha ya wakulima wa mpunga na watanzania wote kwa ujumla kwani anaamini kuwa wakulima wakizalisha kwa tija basi kilio cha maisha magumu na kupanda kwa gharama za maisha itakuwa ni ndoto kwao.
Subscribe to:
Posts (Atom)