Fri 10 Aug 7:23AM
Kina mama wavutiwa na kilimo cha umwagiliaji kilombero
|
Thursday, 26 July 2012 10:59
|
MRADI mkubwa wa umwagiliaji katika Kijiji cha Mkula umeonekana kuwaletea manufaa wakazi wa kijiji hicho na vijiji vya jirani baada ya uzalishaji wa mpunga kuongezeka.
Mradi wa umwagiliaji una ukubwa wa hekta 254 na umebadilisha maisha ya wakazi wa vijiji hivyo kwa mfano, njaa sasa itakuwa ni historia.
Mradi huo uko chini ya Mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo wilayani Kilombero (DAADP’S) na umeweza kuboresha maisha ya wakulima hao baada ya mavuno kuongezeka.
Kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo wakulima walikuwa wakivuna magunia matano ya mpunga katika heka moja, lakini sasa wanapata gunia 20 mpaka 25—matokeo ambayo yamewavutia watu wengi hasa vijana kujiingiza kwenye kilimo tofauti na awali.
“Tunaishukuru Wilaya ya Kilombero kwa kutuletea mradi huu kwani suala la njaa kwa sasa halipo pia tuna uwezo wa kuwasomesha watoto bila shida baada ya kuuza mazao yetu,”anasema Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkula, Salehe Semboko.
Mradi huo ambao ulianza mwaka 2005 umewavutia vijana ambao awali walikuwa hawapendi kulima kwa kuwa kazi hiyo haikuwa na faida.
Lakini kuanzishwa kwa mradi huo umebadilisha mtazamo wa vijana na wameamua sasa kuanzisha shughuli za kilimo kwa kuwa wanavuna mazao mengi na kuyauza.
“Hapa kwetu tuna misimu mitatu ya kilimo kwa mwaka ukilinganisha na maeneo mengine, hii imesababisha tujitume zaidi—mpaka sasa asilimia 80 ya vijana wetu wanajishughulisha na kilimo,” anafafanua mkulima kijana, Mohamed Nafulisa.
Wanawake nao hawako nyuma wanasema kipato chao kimeongezeka na wana uwezo wa kuendesha familia zao baada ya mavuno kuongezeka na kufanikiwa kuwasomesha watoto wao bila tatizo. “Kwa kiasi kikubwa mradi huu umetutoa katika umasikini, mimi nilikuwa naishi Dar es Salaam, lakini baada ya kuja huku na kuona wanawake wengine wanavyofaidika na mradi nikaamua kuanza kulima, sasa nasomesha watoto wangu mimi mwenyewe,” mkazi wa Kijiji cha Mkula, Dora Manyema. Pamoja na mradi huo kuboresha maisha ya wakazi wa Mkula bado wakulima hao wanakabiliwa na matatizo mengi kwa mfano kuna baadhi ya maeneo hayafikiwi na maji. Kutokana na kuwapo kwa tatizo hilo hekta 100 tu zinafikiwa maji huku hekta 154 zikiwa hazina maji na kusubiri mvua. Matatizo mengine wakulima wengi hawana pembejeo hasa mbolea ambayo haifiki kwa wakati na kukosa dawa ya kuulia wadudu hivyo kuwapa wakati mgumu wakulima hao.
“Unajua suala la mbolea kuchelewa linatutatiza sana kwa mfano, tunakuwa na mahitaji ya mbolea na pembejeo nyingine Oktoba, lakini zinafika hapa Aprili sasa tutazitumia vipi? Anahoji Semboko.
Tatizo lingine linaloonekana kuwakwamisha wakulima hao ni kutopatiwa mafunzo ya kuaandaa mashamba, kupalilia, kuvuna, kutafuta masoko.
Tatizo la wakulima kutopatiwa mafunzo—limesababisha wakulima kuuza mazao yao kwa bei ambayo inawanufaisha wafanyabiashara kutokana na madalali kupanga bei zao.
Wakulima hao wanazimika kuuza mazao yao kwa kufuata bei ya madalali kwa sababu hawajui soko la kuuzia mazao yao. Suala la mbolea feki limeonekana kuwatesa wakulima wa Kijiji cha Mkula kutokana na ukweli kwamba wanatumia gharama nyingi kuhakikisha wanapata mbolea kwa ajili ya mavuno yenye tija, lakini wanaambulia kupata mbolea feki ambayo imekuwa ikiharibu mazao yao. “Kwa mfano tulitumia mbolea, lakini baada ya siku chache mazao yalibadilika rangi na kuwa njano tupu na kudhoofika, kwa sasa tunataka mbolea ikabidhiwe kwetu moja moja, kuliko mbolea kupitia kwa mwakala,” anaelezea Dora Abdallah. Kukosekana kwa mashine ya kukoboa imekuwa tatizo kubwa kutokana na kuwapo kwa mashine chache na wakulima wamekuwa wakitumia gharama kubwa na muda mwingi kufuata huduma hiyo mbali na kijiji hicho. Wakulima hao wanaamini kwamba kama wafanyabisahara watafunga mashine za kukoboa wataweza kukoboa mchele na kuuza na thamani ya bidhaa hiyo kuongezeka. “Kama wawekezaji watajitokeza na kuwekeza kwenye pembejeo itasaidia kuongeza uzalishaji, pia naamini watu wengine watatamani kushiriki katika kilimo kwani kwa sasa kilimo ni biashara,” anasema Abdallah. Wakulima wanaiomba Serikali, taasisi binafsi na wadau mbalimbali kuiangalia Kijiji cha Mkula kwa jicho la tofauti kwa kuwa wanaamini kama matatizo ya pembejeo, masoko yatatatuliwa, ghala la chakula la Taifa litapata chakula kingi kutoka katika kijiji hicho. “Siyo maeneo mengi yana uwezo wa kuzalisha kwa misimu mitatu, lakini hapa kwetu hilo linafanyika basi ni wakati mzuri wa kuweka utaratibu mzuri wa kutufikishia pembejeo kwa wakati. Wakulima hao wanashauri kwamba wanaoshughulikia masuala ya pembejeo wanapaswa kuzungumza na wa wakulima hao ili kujua mahitaji yetu,” anasisitiza mwenyekiti wa Kijiji cha Mkula, Semboko. Wakulima wa kijiji hicho wanabainisha kwamba kutokana wao kufanikiwa kuzalisha mpunga kwa misimu mitatu, wakulima wa maeneo mengine wanapaswa kujifunza mengi kutoka kwao ili wafanikiwe katika kilimo cha mazao mbalimbali.. |
No comments:
Post a Comment